KAMATI YA BUNGE YAPITISHA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 ambayo yanahusisha na Taasisi zilizo chini yake.
Kamati hiyo imepitisha makadirio hayo katika kikao kilichofanyika leo Machi 22, 2024 jijini Dodoma ambapo Wizara imewasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameieleza Kamati hiyo kuhusu mikakati na mipango mbalimbali ambayo Wizara imepanga kuitekeleza katika Mwaka wa Fedha 2024/25 ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa na maendeleo ya taifa kupitia rasilimali madini.
Mavunde ameainisha baadhi ya mikakati kuwa ni pamoja na kufanya utafiti wa kina wa madini ili kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia 16 ya sasa kupitia Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri pamoja na kulifanya eneo la Buzwagi Kahama kuwa eneo maalum la uwekezaji.
‘’Mhe. Mwenyekiti, tayari tumefanya majaribio ya urushaji wa ndege nyuki katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo Dodoma, Kahama, Geita na Mirerani. Mirerani tumefanya ndani na nje ya ukuta na hivi karibuni tutarudia tena ndani ya ukuta. Lakini Mwenyekiti, katika Mwaka ujao wa Fedha tumepanga kutumia helkopita kufanya shughuli za utafiti na kupima maeneo mbalimbali ya nchi yetu,’’ amesisitiza Waziri Mavunde.
Ameongeza kwamba, kupitia dira hiyo, Wizara imepanga kuwafikia vijana ili waweze kushiriki katika uchumi wa madini kupitia program ya Mining For Better Tommorow (BMT) ambapo kwa kuanzia, tayari Wizara imeanza mchakato wa kushirikiana na Kampuni ya GF Track kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kuwawezesha kupata vifaa vya kufanyia kazi, suala ambalo litakwenda kwa awamu.
Vilevile, Waziri ameieleza kamati hiyo kuhusu mpango wa Wizara kuongeza idadi ya mitambo ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kueleza kuwa, ifikapo Juni mwaka huu, itaongeza tena mitambo mingine 10 ambayo itasambazwa nchi nzima kwa kanda.
Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Augustine Ollal amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 ambapo ametaja mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa kwa mwaka husika na kueleza kuwa kumekuwa na ongezeko la Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa kwa robo ya Julai- Septemba 2023 kufikia asilimia 10.9 ikilinganishwa na asilimia 9.5 kipindi kama hicho mwaka 2022.
Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini ambapo katika kipindi cha robo ya tatu (Julai hadi Septemba, 2023) ukuaji wa sekta ulifikia asilimia 10.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 9.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2022;
Akizungumzia hali ya makusanyo, amesema makusanyo ya maduhuli yaliyokusanywa na kuwasilishwa Hazina kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024 yameongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 486.30 ikilinganishwa na shilingi bilioni 457.23 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23.
Olla ameyataja mafanikio mengine kuwa ni ununuzi wa mitambo mitano (5) ya uchorongaji (rig) kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo; Kudhibiti vitendo vya utoroshaji na biashara haramu ya madini ambapo Wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 2.42; na
‘’ Mhe. Mwenyekiti, Jumla ya leseni 8,480 zimetolewa katika shughuli za madini kati ya leseni 6,920 zilizopangwa kutolewa katika kipindi husika,’’ amesema Ollal.
Kwa upande wake, Kamati hiyo imeipongeza Wizara kutokana na mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na pia imempongeza Waziri kwa kutoa maelekezo ya kufutwa kwa jumla ya leseni 2,648.