“EPUKENI UTAMADUNI WA KUWAOGOPA VIONGOZI” WAZIRI PROF. KITILA

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo kutokuwa na Utamaduni wa kuwaogopa Viongozi na badala yake wanapaswa kuwaheshimu na kuzingatia misingi ya Utawala Bora bila kuvunja Sheria.

Waziri Prof. Kitila ametoa maagizo hayo mapema leo 22, machi 2024 Jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.

Amesema Viongozi wanaheshimiwa na sio kuogopwa na kukiwa na Taasisi ambayo inawaogopa Viongozi ni hatari zaidi kwani kutakuwa na watu wachache wanaotoa mawazo.

“Epukeni kwa haraka sana Utamaduni wa kuwaogopa Viongozi. Mimi sipendi kuogopwa na hata Katibu wangu hapendi kuogopwa. Viongozi wanaheshimiwa hawaogopwi, kama mnaheshimiana kila mtu anashiriki kwenye kutoa mawazo ya kujenga Taasisi, una uwezo wa kusema Kwa heshima yako Mheshimiwa Waziri kutokana na ufahamu wangu hili jambo sio sahihi” Amesema Waziri Prof. Kitila

Aidha, amesisitiza kufanya mambo kwa kuzingatia Misingi ya Utawala Bora kwa kufuata sheria, Kanuni na taratibu na kuhakikisha wanakuwa na Maarifa pamoja na kujifunza na kuepuka kuwasaidia Viongozi kuvunja Sheria

“Usije ukamsaidia Kiongozi kuvunja Sheria, kuna wataalamu hata kama Kiongozi amesema yeye atatafuta uhalali wa kufanya hilo jambo hata kama anajua linavunja Sheria na Kuna wataalamu wetu wanaona ni jambo la maana sana kutekeleza maelekezo ya Kiongozi kuliko Sheria hata kama maelekezo hayo yanavunja Sheria.

Ametolea Mfano wakati akiwa Katibu Mkuu aliwahi kuwatega wataalamu kwa Kuandika dokezo kwa kujua ni kinyume na sheria na kisha akaitisha Kikao cha menejimenti kwaajili ya kujadili utekelezaji wake ndipo Mkurugenzi mmoja tu aliyesimama na kusema limevunja Sheria.

“Nikawaambia mlitaka kunisaidia kuvunja Sheria, hiyo ni mbaya sana. usimsaidie Kiongozi kuvunja Sheria halafu baadae unaanza kujutia kwanini haujatoa Ushauri” amesisitiza Prof. Kitila

Katika hatua nyingine amewaasa kuacha Tabia ya kutafuta vyeo na badala yake waache vyeo viwatafute kwani mambo hayo yanaendana na wakati pamoja na bahati.

Kwa Upande mwingine Waziri huyo amewataka kufanya kazi kwa ushirikishwaji bila kuangalia madaraja bila kusahau kuwa na Upendo bila kuoneana Choyo.

Amesisitiza, ili hayo yote yafanikiwe ni kuhakikisha unafanya Kazi kwa Maarifa, Bidii na welevu ili kupata matokeo

Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mhe. Waziri, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amesema kuwepo kwa Baraza hilo ni mhimu katika kuleta ufanisi na mahusiano mazuri kazini kwani kutakuwa na ushirikishwaji kwa watumishi kwani wanayo haki ya Kushiriki katika mambo yanayohusu Kazi, haki zao za utumishi na maslahi yao kwa kutumia wawakilishi wao katika Vyama vya wafanyakazi.

“Kila mtumishi anahimizwa kutoa Mchango wa mawazo kwa lengo la kuongeza tija na kutoa huduma Bora” amesema Dkt. Kida

Ameeleza kuwa Baraza hilo litasaidia kusimamia vyema maslahi na stahili za watumishi, pia kuishauri Ofisi kuhusu namna nzuri ya kubuni sera na Mipango ya kuvutia Uwekezaji, Sambamba na kushauriana na mwajiri juu ya ufanisi wa Kazi juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kuhakikisha huduma zitolewazo zinaridhisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *