KAMATI YA BUNGE VIWANDA, BIASHARA KILIMO NA MIFUGO YAPOKEA NA KUJADILI TAARIFA YA UTEKELEZAJI UJENZI WA MNADA HOROHORO
Na. Edith Masanyika, Tanga
Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo leo tarehe 16 Machi, 2024 jijini Tanga wamehitimisha ziara yao ya siku mbili kwa Kupokea na Kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Ujenzi wa Mnada wa Mifugo wa Mpakani wa Horohoro katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga.
Mradi huo ulijumuisha ujenzi wa mazizi 4, kishushio na kipakilio, kiringe, banda la mbuzi lenye uwezo wa kuchukua mbuzi 500, birika la kunyweshea mifugo, kujenga jengo la vyoo vya matundu 6 na kuunganisha mnada na huduma za umeme na maji.
Aidha, Mwenyekiti pamoja na wajumbe waliipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na watendaji wa Halmashauri hiyo kwa ujenzi wa mnada mzuri ambao utachochea ari ya maendeleo ya Halmashauri. Mwenyekiti aliendelea kwa kuwasisitiza kukamilisha ujenzi wa mnada huo ikiwa ni pamoja na kuleta maji mnadani hapo.