KAMATI YA NISHATI NA MADINI YAFANYA ZIARA VITUO VYA GESI DAR ES SALAAM

0

Na: Omary Machunda

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeendelea na ziara yake hii leo ambapo imetembelea vituo vya gesi iliyoshindiliwa (Compressed Natural Gas – CNG Stations) katika eneo la Ubungo Maziwa pamoja na Kituo cha Taqa – Dalbit kilichopo Kipawa Jijini Dar Es Salaam.

Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, Kamati ilipokea taarifa ya uendeshaji wa vituo hivyo iliyowasilishwa na Injinia Aristides Katto kutoka Shirika la maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC).

Taarifa hiyo ilieleza kuwa TPDC inatekeleza mpango wa ujenzi wa vituo vitatu vya CNG katika Jiji la Dar Es Salaam pamoja na mkoa wa Pwani ambapo viitajengwa pembezoni mwa barabara ya Sam Nujomba eneo la Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

Aidha taarifa hiyo ilibainisha uwepo wa ongezeko kubwa la wateja wanaohitaji kubadilisha magari yao kutoka kutumia mafuta ya dizeli na petrol na kutumia gesi asilia ambayo ina gharama nafuu ikilinganishwa na nishati ya petrol na dizeli.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. David Mathayo aliipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kufanya uwekezaji katika sekta ya nishati unaoendelea kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini.

Alisema, “tunajua Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuhakikisha inawekeza katika sekta hii ambayo itawezesha watanzania wengi kupata nishati ya gesi kwa gharama nafuu na kuepukana gharama kubwa za mafuta.”

Naye mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Angelita Mabula aliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya gesi katika mikoa mingine nchini ili kutoa fursa kwa wananchi kunufaika na huduma hiyo ambayo kwa sasa inapatikana katika Jiji la Dar Es Salaam pekee.

Alisema, “matumizi ya gesi asilia iliyosindiliwa kama nishati ya kuendeshea magari bdala ya mafuta ya petroli na dizeli ni nafuu kubwa hivyo Serikali iangalie namna ya kuanzisha vituo kama hivyo katikamikoa mbalimbali hapa nchini ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hiyo”.

Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Joseph Msukuma aliishauri wizara ya nidati kuhakikisha inaanzisha mpango mkakati wa kupunguza gharama za kubadilisha mifumo ya magari ili kuweza kutumia gesi hiyo aambapo huduma hiyo kwa sasa inagharimu kati ya shilingi million moja na laki tano hadi milioni moja na laki nane.

Alisema, “Serikali iangalie namna ya kupunguza gharama za kubadilisha mfumo wa magari kutoka kutumia mafuta ya petroli na dizeli na kutumia nishati ya gesi kwa kuwa gharama za sasa ni kubwa na kufanya watu wengi kushindwa kuzimudu kwa kuwa lengo ni kuwasaidia watanzania kuondokana na adha hiyo”.

Akitoa ufafanuzi juu ya hoja mbalimbali zilizotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo, Naibu Waziri wa nishati Mhe. Judith Kapinga aliahidi kutekeleza ushauri wa Kamati hiyo ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati.

Alisema, tunapokea ushauri wenu waheshimiwa wajumbe wa Kamati hii na tutaifanyia kazi na kwa sasa Serikali ina mkakati wa kushirikiana na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuongeza karakana kwa ajili ya kubadilisha mifumo ya nishati katika magari ili wananchi wengi waweze kupata huduma hii.

Kamati ya Nishati na Madini inaendelea na ziara yake Jijini Dar Es Salaam ambapo itakagua miradi mbalimbali inayotelezwa na Serikali kabla ya kuwasilisha Taarifa yake katika Bunge la Kumi na Tano linalotarajia kuanza siku ya jumanne tarehe 2 Aprili, 2024 Jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *