TANZANIA YAPONGEZWA KWA USTAWI WA ADPA

0

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imepongezwa na Wanachama wa Umoja wa Nchi zinazozalisha Almasi Afrika (ADPA) kwa kusaidia kustawisha Umoja huo wakati ikiwa Mwenyekiti kipindi cha miaka miwili kuanzia 2021 hadi 2023.

Hayo yalielezwa Machi 13, 2024 Mjini Victoria Falls, nchini Zimbabwe na Mkurugenzi wa Biashara ya Madini ya Vito kutoka Wakala wa Taifa wa Madini Nchini Sierra Leone, Mohamed Bah ambaye ni sehemu ya Ujumbe wa Sierra Leone ambao ni Makamu Mwenyekiti wa ADPA wakiisaidia Zimbabwe.

Alisema kuwa, Umoja huo umestawi na kuendelea kuwa na nguvu kutokana na Tanzania kuiongoza ADPA kwa usimamizi na ufuatiliaji thabiti katika miaka miwili ya Uenyekiti ikisaidiwa na Zimbabwe kama Makamu Mwenyekiti. Tanzania ilikabidhi rasmi nafasi ya Uenyekiti kwa Zimbabwe Machi 2023.

Aidha, Bah aliongeza kuwa Nchi nyingi za Afrika Magharibi ziliyumba kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliozorotesha shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na uchimbaji madini na hivyo ushiriki wao kuyumba kutokana na changamoto hizo lakini Tanzania iliendelea kuhamasisha na kuwakumbusha kutimiza wajibu kwa kuwasisitiza kulipia ada za uanachama na kusaidia kuimarisha ADPA.

Akizungumzia pongezi hizo, Kamishna Msaidizi wa Madini – Sehemu ya Uendelezaji Uchimbaji Mdogo na Mratibu wa ADPA Tanzania, Francis Mihayo alisema kuwa matokeo hayo yalitokana na maagizo ya Viongozi wa Wizara wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Madini ambaye hivi sasa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa ADPA kipindi hicho.

Vilevile, Mihayo aliongeza kuwa ni jambo la kujivunia kama taifa kutambulika kwa mchango wake katika ustawi wa Umoja huo na kwamba lengo la Tanzania ni kuona malengo ya kuanzishwa ADPA yanafikiwa.

Mkutano wa Tisa wa Wataalam na Baraza la Mawaziri wa ADPA unaoendelea mjini Victoria Falls, nchini Zimbabwe ambapo unatarajiwa kuhitimishwa leo Machi 14, 2024.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa ADPA unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo akiambatana na Kamishna Msaidizi wa Madini- Sehemu ya Uendelezaji Uchimbaji Mdogo ambaye pia ni Mratibu wa ADPA Tanzania, Francis Mihayo pamoja na Afisa Tawala Henry Shadolo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *