MAVUNDE AIHAKIKISHIA KAMATI YA BUNGE KUUFANYIA KAZI USHAURI UJENZI JENGO LA TGC

0

Litahusisha Madarasa, Mabweni ya wanafunzi, Viwanda vya Kuongeza Thamani Madini, Makumbusho ya Madini, Maduka ya bidhaa za Madini

Arusha

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa Wizara itaufanyia kazi ushauri uliotolewa wa kuhakikisha Mradi wa Jengo la Ghorofa Nane la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) linakidhi Mahitaji ya Watumiaji kwa kipindi kirefu.

Ameyabainisha hayo Machi 13, 2024 wakati wa ziara ya Kamati hiyo ilipotembelea eneo linapotarajiwa kujengwa jengo la ghorofa nane (8) la TGC kilichopo Kata ya Themi-Njiro, Jijini Arusha ikiwa ni sehemu ya utanuzi wa miundombinu ya Kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Madini kinachojihusisha na utoaji mafunzo ya uongezaji thamani madini yakihusisha ukataji na ungarishaji wa madini ya vito; utambuzi wa Madini ya Vito; na utengenezaji wa bidhaa za usonara kama Pete, hereni, mikufu, n.k. pamoja na HUDUMA mbalimbali kama maabara ya Madini ya vito.\

‘’Tutazingatia ushauri mzuri uliotolewa na Kamati ili ujenzi wa jengo hilo utakapo kamilika uwe wa kiwango Cha kimataifa na kukidhi mahitaji ya watumiaji kwa kipindi kirefu ikizingatiwa kuwa eneo litakapojengwa jengo hilo ni nyeti, lipo karibu na mjini na rahisi kufikika,’’amesema Waziri Mavunde.

Waziri Mavunde amezitaja huduma zitakazokuwa ndani ya jengo hilo na kusema kuwa ni pamoja Ofisi za TGC, Ofisi za Madini kwa Mkoa wa Arusha, Viwanda vya uongezaji thamani madini vya wafanyabiashara, sehemu maalum ya kuendesha minada ya madini, maktaba pamoja na mabweni ya wanafunzi watakaojiunga na kituo hicho.

Amezitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na maabara za Madini ya Vito na bidhaa za usonara, makumbusho ya Madini ya Vito na bidhaa za sonara na maduka ya bidhaa za Madini.

Ameongeza kwamba, upanuzi wa miundombinu ya kituo hicho ni mojawapo hatua za utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na mikakati ya muda mfupi na mrefu ya Wizara ya kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani Madini kufanyika nchini ikiwemo kuongeza na kuzalisha wataalam katika tasnia hiyo, ambao wataweza kufanya shughuli za uongezaji thamani madini kwa ubora wa kimataifa .

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dkt. David Mathayo ameitaka Wizara kuangalia uwezekano wa kuongeza ukubwa wa eneo ili kukidhi mahitaji ya muda mrefu ya jengo hilo kuweza kupokea na kuhudumia wageni wanaokuja kupata huduma mbalimbali zitakazotolewa ikiwemo maabara za Madini, uendeshaji wa minada ya madini ya vito, mafunzo ya uongezaji thamani madini, n.k.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *