KAMATI YA NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA JENGO LA WIZARA YA NISHATI JIJINI DODOMA

0

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Kilumbe Ng’enda wamekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wizara ya Nishati lililopo katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Kamati ilipokea taarifa ya hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa mradi huo ambapo iliarifiwa kuwa ujenzi umekamilika kwa asilimia 75 na Mkandarasi anatajia kukabidhi jengo hilo kwa Wizara husika ifikapo tarehe 29 Mei, 2024.

Akiongea mara baada ya ukaguzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba aliwahakikishia wajumbe hao kuwa wataalam wake wamekuwa wakifanya kazi kwa weledi kwa kushirikiana na Mkandarasi wa mradi huo ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha mradi huo unakamilika na kukabidhiwa kwa muda uliopangwa.

Alisema, “waheshimiwa wajumbe sisi kama wizara tunafuatilia kwa ukaribu hatua zote za ujenzi wa mradi huu na tumekuwa tukitoa ushirikiano unaohitajika ili mradi huu ukamilike na kukabidhiwa kwetu ndani ya muda ulioainishwa kwenye mkataba tuliosaini na Mkandarasi.”

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko aliwakaribisha wajumbe hao katika Mji huo utakaokuwa Makao Makuu ya Ofisi mbalimbali za Wizara na Taasisi za Serikali na kuwaongoza katika ukaguzi wa jengo hilo.

Alosema, “waheshimiwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini sisi kama wizara tunawashukuru kwa kututembelea, tunawakaribisha mahali hapa mfanye kazi yenu na sisi tupo tayari kupokea ushauri na maelekezo yenu.”

Akiwasilisha ushauri na maelekezo ya Kamati yake Mhe. Ng’enda alipongeza hatua iliyofikiwa katika mradi huo huku akitoa maelekezo ya Kamati hiyo kwa kuitaka Wizara ya Nishati ihakikishe Mkandarasi anarekebisha changamoto zilizojitokeza ili ujenzi ukamilike kwa wakati na kuakisi thamani ya fedha zilizotumika kwenye mradi huo.

Alisema, “zipo baadhi ya changamoto tulizoziona ikiwemo wasiwasi kutoka miongoni mwetu kuwa mradi huu unaweza usikamilike kwa wakati, hivyo ni jukumu lenu kama wizara kuhakikisha changamoto hizo haziathiri ukamilishaji wa mradi kwa wakati ili kuepuka ongezeko la gharama za mradi huu.”

Ziara hiyo iliyoanza hii leo ni sehemu ya Shughuli za Kamati za Kudumu za Bunge katika kutekeleza jukumu la Kuishauri na Kuisimamia Serikali kupitia ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.

Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge zitawasilishwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge maarufu kama Mkutano wa Bajeti utakaoanza tarehe 2 April, 2024 Jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *