SAGINI ASEMA AJALI BARABARANI CHANZO KIKUU CHA VIFO KWA VIJANA WENYE UMRI 5-29

0

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini (Mb) amesema
tafiti zinaonesha watu wengi wanapoteza maisha kutokana na ajali za barabarani huku Vijana ndiyo kundi linaloathirika zaidi, kulingana na Shirika la Afya Duniani, ajali za Barabarani ni chanzo kikuu cha Vifo vya vijana wadogo wenye umri kati ya Miaka 5-29, vifo vinavyoyazidi magonjwa mengine.

Mhe. Sagini aliyasema hayo Machi 6, 2024 alipokuwa akizungumza wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Mkutano wa Bomba la Mafuta ghafi Afrika Mashariki (EACOP) kuhusu Programu ya Usalama wa Raia Barabarani Jijini Dar es Salaam, alisema kuwa, takwimu pia zinaonesha kama hali itaendelea hivi, ajali za barabarani itakuwa chanzo cha vifo vingi duniani kwa watu wa rika zote.

“Nchini Tanzania ajali za barabarani zinaongoza kwa wingi wa vifo na Majeruhi kwa miaka mitatu iliyopita, 2021-2023 na kama suala hili halitapatiwa mwarobaini linaweza kuwa chanzo kikubwa cha vifo nchini Tanzania,” Alisema Mhe. Sagini.

Pia alisema kuwa, Programu ya Usalama wa Raia Barabarani inayotekelezwa na Bomba la Mafuta ghafi Afrika Mashariki kwa msaada wa shirika la AMEND unatoa njia juu ya kujenga miundombinu salama ya barabara na kujenga uwajibikaji na matumizi safi ya barabara ambapo ametaka kuona ushirikiano wa Serikali, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Taasisi za Sekta Binafsi na Jamii kwa Ujumla.

Hata hivyo, Mhe. Sagini alieleza kuwa njia ya Bomba la Mafuta ghafi Afrika Mashariki inaanzia Kabaale – Hoima Nchini Uganda Mpaka Chongoleani, Tanga Nchini Tanzania huku likipita kwenye Mikoa Nane ambayo ni Kagera, Shinyanga, Tabora, Mwanza, Manyara na Kilimanjaro pamoja na Wilaya 38 za Nchini Tanzania hivyo linatatoa manufaa mengi ya kiuchumi nchini Tanzania kama njia kuu ya Bomba hilo lenye urefu wa Kilomita 1, 147 hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuangalia Usalama wa Wananchi wanaoishi kwenye Maeneo hayo ambalo bomba linapita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *