DKT. MSONDE AWATAKA MWALIMU KULETA MAPINDUZI KATIKA ELIMU

0

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amewataka walimu wote nchini kuhakikisha wanaleta mapinduzi katika elimu kwani Serikali inawatengemea katika eneo hilo na ndio kipaumbele kimojawapo cha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa walimu , kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na walimu wa Halmashauri za Wilaya ya Gairo, Kilosa na Mvomero ambao wanahudhuria mafunzo ya walimu wa masomo ya sayansi na kiingereza kwa shule za msingi kupitia siku maalumu ya MEWAKA nchini.

“Mwalimu ukiamua unaweza kufanya mambo makubwa sana katika taifa letu na ndio maana Serikali ya Awamu ya Sita inawategemea katika kuleta mapinduzi ya elimu ambayo ni mojawapo ya kipaumbele cha Mheshimiwa Rais,” Dkt. Msonde amesisitiza.

Dkt. Msonde amesema, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka watoto wa kitanzania wapate ujuzi unaostahili, na kuongeza kuwa Mhe. Rais anatarajia wanafunzi wote wa darasa la kwanza, la pili na la tatu wajue kusoma na kuandika kwa ufasaha.

Dkt. Msonde amesema kuwa, walimu wakiwafundisha vizuri watoto ni dhahiri kuwa watapata umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu ikiwa ni pamoja na umahiri wa masomo yote wanayofundishwa.

“Mnapofundisha lengo lisiwe kumaliza kurasa za vitabu bali mjikite katika kuhakikisha watoto wanapata ujuzi katika somo husika na umahiri ndio jambo la kupewa kipaumbele,” amesema Dkt. Msonde.

Dkt. Msonde ameeleza bayana kuwa, Serikali inawaamini na kuwathamini walimu wote nchini na ndio maana inajali maslahi yao hivyo ni jukumu lao kuamua kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwa mustakabali wa elimu na masilahi mapana ya taifa.

Jumla ya walimu 60,036 nchini wanahudhuria mafunzo ya walimu wa masomo ya sayansi na kiingereza kwa shule za msingi kupitia siku maalumu ya MEWAKA kupitia vituo mbalimbali vilivyopo katika wilaya zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *