TFRA YABAINISHA FURSA ZA UWEKEZAJI TASNIA YA MBOLEA

0

Imeelezwa kuwa, Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta zote za kiuchumi kwa sekta zote za uzalishaji na  tasnia ya mbolea ikiwepo.

Hayo yameelezwa leo tarehe 15 Februari, 2024 na Bw. Daniel Maarifa, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Mashariki akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Bw. Joel Laurent, wakati wa kikao cha mtandaoni (video round table) baina ya wafanyabiashara wa mbolea wa Tanzania na wa nchini Urusi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Utamaduni cha Urusi kilichopo Upanga, Jijini Dar Es Salaam. 

Bw. Daniel Maarifa amesema, kikao hicho ni mwanzo wa mahusiano ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili utakaopelekea kuingizwa kwa tekinolojia mpya kwenye Sekta ya kilimo hususani tasnia ya mbolea na kupelekea tija kuongezeka kwenye Sekta ya kilimo.

Aidha, Maarifa amewahakikishia wafanyabiashara wa Urusi upatikanaji wa malighafi za viwanda kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa madini ya fosifeti ujazo wa tani 375.1, gesi asilia tani za ujazo trilioni 57, uwepo wa makaa ya mawe we ya kutosha, madini ya chokaa na madini mengine yaliyotawanyika katika maeneo tofautitofauti nchini.

Akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa Habari, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan amesema, Tanzania imeonesha uwepo wa fursa za uwekezaji wa viwanda vya mbolea nchini na hivyo kikao hicho kimelenga kuweka daraja baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Urusi ili waweze kuja kuwekeza katika ujenzi wa viwanda Pamoja na kushirikiana kwenye biashara ya mbolea.

Amesema, kwa mtazamo wake kwa namna nchi ya Tanzania na nchi Jirani za Afrika Mashariki zilivyo, fursa zipo nyingi sana za kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea na kueleza ubalozi wake utaweka nguvu kubwa katika kuhakikisha mahusiano haya ya kibiashara baina ya Tanzania na Urusi yanafikiwa.        
                                              
Kwa upande wake, Elizabeth Muzo, Afisa Uhamasishaji na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ametoa mwaliko kwa wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kueleza uhakika wa kuwafikia watu milioni 400 kwa Tanzania na kwa soko la nchi zilizopo chini ya jangwa la Sahara takribani zaidi ya watu milioni 600.

Aidha, Muzo ameeleza kuwa, kupitia ofisi yake, Tanzania iko radhi kutoa ardhi kwa ajili ya kufanikisha uwekezaji wao ikiwa ni pamoja na kutoa misamaha ya ushuru wa forodha kwenye mitambo na mashine za viwandani..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *