STAMICO YAIHAKIKISHIA SHANTA MINING HUDUMA BORA YA UCHORONGAJI

0


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse ameiahidi Kampuni ya Shanta Mining kuwapatia huduma bora ya uchorongaji katika mradi wao wa Singida Gold Mine na kwamba uamuzi wa kuchagua Shirika hilo ni sahihi na hawatajutia.

Amesema hayo leo Februari 16, 2024 wakati wa hafla fupi ya utiaji saini Kandarasi ya Uchorongaji kati ya STAMICO na Shanta Mining iliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema kuwa tukio hilo ni sehemu ya mageuzi ambayo Shirika hilo linaendelea kufanya katika ushiriki wake kwenye mnyororo mzima wa shughuli za Uchimbaji na Utafiti wa Madini ambao inahusisha uchorongaji na kwamba Kandarasi hiyo kwa STAMICO ina maana kubwa zaidi kwa kuingia Kanda ya Kati baada ya kufanya shughuli ya uchorongaji kwa Kanda ya ziwa katika migodi mikubwa ikiwemo Geita Gold Mine, Buckreef, Buhimba na sasa kanda ya kati.



“Kandarasi hii tumesaini mbele ya umma, nikuhakikishie kwamba tunakwenda kukupa huduma bora, tunaamini kwamba umefanya uchunguzi wa kutosha kujua uwezo na utaalamu wetu kule ambako tayari tunachoronga na kuamua kufanya huu uamuzi huu, shirika linawahakikidhia kuwa hamjafanya uamuzi wa makosa na mmefanya uamuzi sahihi, kwasababu tumeonyesha uzoefu wetu tayari na Wataalam tunao, tunazo mashine za kisasa za kuchoronga na nyingine zinakuja” amesema Dkt. Mwasse.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mgodi wa Singida Gold Mine, Mhandisi Honest Mrema amesema kuwa Kampuni hiyo imeamua kuingia kandarasi hiyo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 1.08 sawa na shilingi bilioni 2.7 na STAMICO kwa kuwa wanahitaji mashine za kisasa kwa ajili ya uchimbaji na kuendelea kufanya utafiti katika eneo lao wanalomiliki leseni na hatimaye kufikia lengo la kuwa mgodi wa kati kwa kuchoronga sana mwaka huu na ujao ili kuupanua Mgodi wa huo Dhahabu wa Singida.


“Kwa historia yenu tuliyosikia hizi mita 5000 ni za kuanzia tu, tunaweza tukaongeza kiasi kutoka kwenye hizo dola bilioni 1.08 na kuwa mara tatu zaidi kutoka na matokeo ya kufanya vizuri kwasababu maeneo tunayo, pia tunaamini huu ushirikiano ni wa muda mrefu sio wa miezi 6 tu kama tulivyosaini hapa, kama Mungu akijaalia bei ya dhahabu duniani ikaendelea kuwa nzuri basi tutaendelea kuwekeza kwenye utafiti zaidi ili kuongeza uzalishaji zaidi, kwa pamoja tutafika mbali” amesema Mhandisi Mrema.

Kampuni ya Shanta Mining inamiliki Mgodi wa Dhahabu wa Singida uliopo wilayani Ikungi mkoani Singida wenye hadhi ya mgodi wa kati na ulianza shughuli za uzalishaji mwezi Machi 2023.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *