BENKI YA AZANIA NA SHIRIKA LA NYUMBA ZANZIBAR WAJA NA MIKOPO YA NYUMBA NAFUU

0


Benki ya Azania kwa kushirikana na Shirika la nyumba Zanzibar (ZHC) leo Februari 14,2024, wamezindua huduma ya mikopo ya nyumba zilizojengwa na Shirika hilo maeneno mbalimbali jijini Unguja na Pemba. Hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo imefanyika katika tawi la Benki ya Azania-Zanzibar.

Akiongea katika hafla hiyo iliyoambatana na utiaji saini wa makubaliano baina ya Benki ya Azania na ZHC, Meneja Mwandamizi wa wateja Binafsi wa Benki hiyo Bw. Jackson Lohay alisema kuwa Benki hiyo imejipanga na iko tayari kuwakopesha watakaohitaji nyumba hizo ambazo gharama zake ni nafuu sana.

“Kwanza kabisa niwapongeze ZHC kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na sisi, katika hili wameonesha uhalisia wa kuwa ni shirika ambalo linalenga kumuinua mzanzibari kwa vitendo,” alisema Bw. Lohay huku akiongeza kuwa Benki hiyo ndio Benki ya kwanza nchini Tanzania kukopesha mikopo ya nyumba.

“Sisi Benki ya Azania tuko tayari kuwahudumia kwani hatuna ugeni kwenye biashara hii, tuna uzoefu wa kutosha kama ambavyo nimeeleza na tutawakopesha kwa riba ya chini sana ya kuanzia asilimia 14% (Reducing) tu ambapo muda wa marejesho ni mpaka kufikia miaka 25 na masharti yake ni nafuu sana. Mtanzania yeyote anaruhusiwa ili mradi awe anakidhi vigezo na masharti ya kuweza kurejesha kulingana na mtiririko wa malipo”.

Kwa upande wa Shirika la ZHC, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Bi. Mwanaisha Ali Said alisema kuwa makubaliano ambayo wameingia na Benki ya Azania yatawapa urahisi Zaidi wateja wao na sasa watakuwa na wigo mpana wa kuwawezesha kununua na kumiliki nyumba bila hofu.

‘’Kuingia kwa makubaliano haya ni muendelezo wa mipango yetu kama shirika ya kuwawezesha Wazanzibari kununua nyumba kwa njia rahisi, nyumba zetu huwa tunaziuza kwa njia kadhaa ikiwemo fedha taslimu na pia kwa njia ya mkopo yaani Mortgage, baada ya kuona ununuzi kwa njia ya mkopo hatujafanya vizuri sana ndipo tuliwafuata Benki ya Azania kwa kuwa tunafahamu wao wana uzoefu mkubwa eneo hilo la Mortgage Financing na hatimaye leo tunatiliana saini makubaliano rasmi’’.

‘’Niwasihi wananchi wote kuchangamkia fursa hii, kwa sasa tuna mradi wa eneo la Mombasa Kwa Mchina hapa Zanzibar wa ujenzi wa nyumba 72 ambapo takriban 90% zimeshanunuliwa, lakini pia kuna miradi mingine kama wa eneo la Mfikiwa, Chakechake kule Pemba nyumba 220, Nyamanzi hapa Zanzibar nyumba 120 na Kisakakasaka nyumba 240’’, alimalizia Bi. Mwanaisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *