BASHUNGWA AITAKA TANROADS KUPATA SULUHU YA BARABARA KUHARIBIKA KABLA YA MUDA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutafuta ufumbuzi kuhusu suala la kuharibika kwa barabara kabla ya muda uliopangwa ili kuokoa fedha za Serikali zitakazotumika kurekebisha miundombinu hiyo.
Agizo hilo amelitoa jijini Dodoma Februari 14, 2024 katika kikao cha 19 cha Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS na kuwasisitiza kusimamia miradi kwa weledi na uzalendo ili kusaidia miradi kukamilika kwa viwango na kwa wakati.
“Suala la kuharibika kwa barabara kabla ya wakati ‘pre-mature failure’ ni tatizo, hakikisheni mnapambana nalo, chukueni hatua za kisheria kwa Mkandarasi atakayetekeleza mradi chini ya kiwango”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameagiza TANROADS kutumia kikamilifu mtambo wa Ukaguzi wa Barabara (Road Scanner) wakati wa kufanya ukaguzi wa miradi ya barabara na madaraja na hata kutumia vifaa vingine vitakavyoweza kuwasaidia kubaini ubora wa mradi mapema kabla ya kukabidhiwa.
Ameielekeza TANROADS kuimarisha na kukijengea uwezo Kitengo chake cha Usimamizi wa miradi (TECU), ili kusimamia miradi kwa weledi na ufanisi.
Kadhalika, Bashungwa ameitaka TANROADS kusimamia sheria ya uzito wa magari barabarani na kutoa faini au adhabu nyingine kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo kwa mujibu wa sheria pamoja na kuwaelekeza Maafisa wanaofanya kazi kwenye mizani kutii na kufuata sheria kama inavyoelekeza ili kuzilinda barabara nchini.
“Hakuna kiongozi wala mtumishi ambaye yupo juu ya sheria, hata mimi siwezi kumsaidia yeyote anayekiuka sheria hii, atakayekiuka achukuliwe hatua na sio kunipigia simu”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amesisitiza umuhimu wa Wakala huo kuwajengea uwezo Wataalam wake ikiwemo katika eneo la usimamizi wa miradi na mikataba ili kuleta tija kwa TANROADS na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, amemhakikishia Waziri Bashungwa kutekeleza maagizo aliyowapa na kuendelea kufanya kazi kwa ari na bidi katika utendaji wao wa kila siku ili kuleta tija kwa Wakala huo.
Naye, Mweyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na kazi nyingine (TAMICO), Eng. Nchama Wambura, amesema wataendelea kushrikiana na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya na maendeleo kwa utekelezaji sahihi na ubora kwa miradi wanayoendelea kutekeleza nchini.
Mkutano wa 19 wa Baraza la wafanyakazi la TANROADS, umefanyika Dodoma kwa siku 2 na kushirikisha zaidi ya wajumbe 100 kutoka Mikoa yote nchini.