DKT. DIALLO AITAKA TFRA KUELIMISHA UMMA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA

0

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania amelitaka Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka hiyo kujadili namna bora ya kutoa elimu ya mbolea kwa umma ili kuondoa fikra potofu kuwa mbolea inaharibu udongo.

Amesema, makadirio ya kiasi cha mbolea kinachohitajika kwa mwaka yatabadilika kutokana na elimu ya matumizi sahihi ya mbolea itakayotolewa kwa wananchi ambao baada ya mafunzo wataona umuhimu wa kutumia mbolea na kuongeza tija kwenye kilimo chao.

Ametoa wito huo leo tarehe 13 Februari, 2024 akifungua kikao cha nne  cha baraza la wafanyakazi kinachofanyika katika ukumbi wa Gairo ndani ya hoteli ya Morena mjini Morogoro.

Aidha, amewataka wajumbe wa baraza hilo kujadili vyema makadirio ya bajeti ya mwaka 2024/2025 ili kuhakikisha inaendana na malengo ya Mamlaka.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa Bodi yake itahakikisha Mamlaka inatekeleza majukumu yake kulingana na malengo iliyojiwekea huku ikifuatilia taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka kila robo ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu yake.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza, Bi. Happiness Mbelle Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti alimshukuru Mwenyekiti wa Bodi kwa kutenga muda na kufika kufungua kikao hicho.

Alieleza kuwa Mamlaka imepokea maelekezo, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi kwa maslahi ya Mamlaka na Taifa kwa ujumla.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka na Mwenyekiti wa kikao cha Baraza, Bi. Victoria Elangwa amesema kikao hicho ni jukwaa rasmi la kutoa maoni na mapendekezo yanayoweza kuisaidia Mamlaka kutimiza malengo yake.

Mwisho amewataka wajumbe kutekeleza lengo la kuja kushiriki kikao hicho na kutoa mapendekezo mazuri kwa bajeti inayoendelea kutekelezwa juu ya namna bora ya kuhakikisha kazi zilizopangwa zinatekelezeka.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), akizungumza na wajumbe wa Baraza wakati akifungua kikao cha nne cha Baraza la wafanyakazi la TFRA tarehe 13 Februari, 2024 mjini Morogoro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo (wa pili kutoka kulia) akipokelewa na Kaimu Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa TFRA, Bi. Victoria Elangwa (wa kwanza kulia) alipokuwa akiwasili kwa ajili ya kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa Gairo katika hoteli ya Morena tarehe 13 Februari, 2024
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo (katikati) akiwa katika picha na viongozi wa Tughe tawi la TFRA, Mwakilishi kutoka TUGHE Makao Makuu, TUGHE Mkoa wa Dar Es Salaam na ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, vijana na Ajira. Kushoto kwa Mwenyekiti ni Kaimu Mkurugenzi wa TFRA na Mwenyekiti wa kikao cha Baraza Bi. Victoria Elangwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *