TUMELENGA KUIFANYA TANZANIA KITOVU CHA MADINI AFRIKA – MAHIMBALI
▪︎Zambia Yafurahishwa na Utaratibu wa Wizara Kukutana na Wawekezaji Kila Robo Mwaka
Capetown
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema Tanzania imelenga kuwa Kitovu cha Madini Barani Afrika sababu ambayo imepelekea Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini.
Ameongeza kwamba, Wizara imeweka utaratibu wa kukutana na kampuni kubwa na za kati zilizowekeza katika miradi ya madini nchini kila robo ya mwaka ili kujadili na kutatua kero ambazo zinaweza kusababisha ucheleweshaji wa masuala yanayohusu uwekezaji na kuongeza kuwa, tayari wizara imekwishateua maafisa maalum ambao ni mabalozi wa kila mradi hiyo.
Mahimbali ameyasema hayo Februari 6, 2024 wakati akichangia katika mdahalo maalum uliolenga kujadili ufunguaji wa fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini na namna ya kukabiliana na changamoto zinazopelekea kukwamisha uendelezaji wa miradi mikubwa ya madini katika nchi za Afrika, kwenye mkutano wa Uwekezaji wa Mining Indaba unaoendelea nchini Afrika Kusini.
Akizungumza katika mdahalo huo, mmoja wa wachangiajia katika mdahalo huo kutoka Ofisi ya Rais ya Serikali ya Jamhuri ya Zambia Jito Kayumba, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha utaratibu wa kukutana na wawekezaji na kuongeza kuwa, Tanzania imekuwa mfano kwa nchi hiyo kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa sekta ya madini na kuziasa nchi nyingine kujifunza pale wanapoona kuna jambo la kipekee kutoka sehemu nchi nyingine.
Kwa nyakati tofauti viongozi wakuu wa wizara, wamekutana na kampuni mbalimbali zilizowekeza nchini pamoja na kampuni kadhaa zinazoshiriki katika mkutano huo ambazo zinakutana na Wizara ili kuendelea kupata taarifa za kina zinazohusu uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini.
Kampuni ambazo leo zimekutana na viongozi wa Wizara ni pamoja na MANTRA Tanzania, Tesla, AngloGold Ashanti, BHP na Life Zone Metals, Taasisi ya Jiolojia ya Uingereza na kampuni ya JOGMEC ya Botswana.
Aidha, vikao hivyo vimetanguliwa na kikao kilichohusisha Chemba ya Migodi Tanzania, kampuni zilizowekeza nchini pamoja na kampuni zilizovutiwa na taarifa za uwekezaji za Tanzania.