SIO KWAMBA TUNAMPAMBA RAIS, BALI TUNAMSHUKURU KWA MAKUBWA ANAYOTUFANYIA-MBUNGE DKT. CHAYA

0

Na. Emmanuel Charles-Manyoni Singida

AKABIDHI VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA MILIONI 300 KITUO CHA AFYA SANZA

Baada ya ujenzi wa Kituo cha Afya Sanza kukamilika na kuanza kutoa huduma, hatimaye Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa Vifaa Tiba vyenye thamani ya Tsh. Milioni 300 kwaajili ya kutoa huduma katika Kituo hicho.

Vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na Vitanda, magodoro, jokofu, mashuka na vifaa vingine vya Kisasa ambavyo vimekabidhiwa leo Februari 06, 2024 na Mbunge wa Manyoni Mashariki Mhe. Dkt. Pius Chaya katika Kituo hicho cha Afya cha Sanza, Wilayani Manyoni Mkoani Singida.

Ujenzi wa Kituo hicho umegharimu zaidi ya Milioni 500 hadi kukamilika kwake

Akiwahutubia wananchi wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mbunge Dkt. Chaya amesema kukamilika kwa Kituo hicho ni mafanikio makubwa kiasi ambacho kimepelekea Rais Dkt. Samia kutoa fedha kwaajili ya Vifaa Tiba vya kisasa jambo ambalo hapo awali halikuwahi kutokea
“Rais wetu msikivu sana, ametoa vifaa vya milioni mia tatu, haijwahi kutokea Kituo mnapewa Milioni Mia tano ndani ya Miaka miwili, halafu ndani ya miezi sita mnapewa milioni mia tatu mnunue vifaa vyote vya kisasa.mmewahi kuona wapi? Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, anataka kina Mama, watoto wadogo, wazee na watu wasiojiweza huduma zote wapate hapa, sio kwamba tunampamba , kuna watu nimewaona kwenye kundi moja wanasema mnampamba Rais, watuambie wapi na lini iliwahi kutokea kama hiki kilichofanyika” amesema Dkt. Chaya

Ameeleza kuwa Rais Samia amewajali watu wa Sanza kwani hapo awali watu walikuwa wanapata shida tofauti na sasa watapata huduma zote bila kusafiri kwenda mbali kupata huduma.

Katika hatua nyingine, Mbunge huyo ameahidi kukamilisha ujenzi wa Daraja la Sanza ambalo ni kilio cha muda mrefu na kusema anataka kuacha alama kwa kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo ambalo hata Rais Samia alitoa ahadi wakati wa Ziara yake Mkoani Singida ambapo akihutubia wananchi wa Itigi alimwagiza Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa kuhakikisha Daraja linajengwa

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Dkt. Furaha Mwakafwilwa amewaasa akina Mama kuhakikisha wanakwenda Hospitali mara wanapokaribia kujifungua na kuachana na tabia ya kujifungulia majumbani au kusubiri mpaka wapate uchungu ndipo waende kwenye Kituo cha Afya.

Amebainisha kuwa changamoto mbalimbali zinazotokea kwa upande wa watoto ikiwemo kuzaliwa wakiwa na mapungufu inasababishwa na wazazi kutokuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya na kupelekea watoto kukosa Afya Bora tangu wakiwa tumboni
“haitakuwa na maana Rais anajenga vituo vya Afya, analeta Vifaa tiba vya kisasa halafu bado watu washindwe kufika kupata huduma, nawaombeni mzingatie ushauri wa madaktari na si vinginevyo”

Kwa upande wao wananchi wameeleza kufurahishwa na Huduma mbalimbali wanazopelekewa na Serikali na kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Mbunge wao Mhe. Chaya
Wakizungumza baadhi ya akina Mama wamesema
“Kwakweli tunashukuru sana mbunge wetu kwa kutujengea Kituo cha Afya na kutuletea Vifaa tiba kwani tulikuwa tunahangaika tunaenda mbali kule, saa zingine mvua zinanyesha watu tunashindwa kupita wanajifungulia njiani lakini kwa sasa tunashukuru”

Mbali na kununuliwa kwa Vifaa tiba hivyo, lakini bado imebainishwa kuwa Serikali itatoa fedha zingine kwaajili ya kuongeza Vifaa tiba vingine katika Kituo hicho cha Sanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *