RC MAKALLA AIKARIBISHA NSSF KUWEKEZA KATIKA UWANJA WA NDEGE WA MWANZA

0

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Amos Makalla, ametangaza fursa mbalimbali zinazopatikana katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza huku akiualika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa mbia muhimu wa uwekezaji katika uwanja huo.

Mhe. Makalla amesema hayo leo tarehe 5 Februari, 2024, wakati alipofanya kikao na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Bw. Mussa Mbura, Makao Makuu ya NSSF, Jijini Dar es Salaam.

Aidha, amezitaja fursa za uwekezaji katika uwanja huo kuwa ni kuuendeleza uwanja huo kwa kuboresha jengo la abiria lililopo, pia kujenga jengo kubwa la abiria ambalo litakuwa na hadhi ya kimataifa, kuboresha njia ya kutua na kuruka ndege, kuboresha mfumo wa taa za kuongozea ndege pamoja na kujenga hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano.

Mhe. Makalla ameushukuru Mfuko kwa kuonesha nia hiyo pamoja na TAA kwa kuwa tayari kuwakaribisha NSSF katika uwekezaji na kuona utayari wa taasisi hizi mbili za Serikali kufanya kazi kwa pamoja ili kukuza Uchumi na kuleta maendeleo.

“Tunawakaribisha wadau wengine kwa sasa kipaumbele tumeanza na NSSF kwa sababu tayari wameshawekeza katika mradi wa jengo la hoteli ya nyota tano na sisi mkoa wa Mwanza tunawashukuru kwa sababu tuna mkakati wa kukuza utalii katika jiji letu, pamoja na mambo mengine NSSF tayari wameonesha nia ya dhati ya kuendelea kuwekeza katika mkoa wa Mwanza” amesema Mhe. Makalla.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba alimshukuru Mhe. Makalla kwa kuwa na kikao na taasisi hizo ambacho kimezungumzia mambo mbalimbali ikiwemo kutoa kipaumbele kwa NSSF kuwa mwekezaji mkuu katika kuendeleza uwanja wa ndege wa Mwanza.

“Tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameendelea kufungua nchi na kutuletea fursa za wawekezaji ambao kwetu sekta binafsi ni sekta muhimu kwa kuandikisha wanachama na kukusanya michango” amesema Mshomba.

Amesema NSSF kwa kushirikiana na TAA watafikia hatua ya makubaliano na hatimaye waendelee katika hatua ya utekelezaji kwa maeneo ambayo wameyabainisha  ambayo yataleta faida katika uwekezaji wa mradi huo kwani lengo ni kujenga uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Mussa Mbura amesema Mamlaka hiyo imewasilisha fursa mbalimbali kwa NSSF ili waweze kushirikiana kuwekeza katika uwanja wa ndege wa Mwanza.

Amesema TAA pia inamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiagiza kufanya maboresho katika uwanja wa ndege wa Mwanza kwani tayari fedha kwa ajili ya maboresho hayo zimeshafika na hivi punde wataanza ukarabati wa jengo hilo.

Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa ambayo iko karibu na mbuga za Wanyama, ikiwemo mbuga kubwa zaidi Serengeti, kupitia Mwanza ambapo  inamchukua mtalii saa moja awe ametoka nje ya nchi au ndani ya nchi na kwenda Serengeti kutalii na kurudi Mwanza. Mkoa wa Mwanza ni moja ya mkoa nchini Tanzania ambao una shughuli nyingi sana za kiuchumi ikiwemo uvuvi, kilimo, madini, utalii na biashara, hivyo kuwepo na mzunguko mkubwa wa watu na kupelekea uwanja wa ndege wa Mwanza kuwa na watumiaji wengi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *