TANZANIA YATOA UZOEFU WAKE KUENDELEZA MADINI MKAKATI

0

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa  amepata fursa ya kuelezea  uzoefu wa  Serikali ya Tanzania katika Uendelezaji Madini  Muhimu na Mkakati  na kutoa Wito kwa Nchi za Afrika  kuona umuhimu wa kuwa na  Sera ya Pamoja  kusimamia madini ili Bara la Afrika linufaike ipasavyo.

Dkt. Kiruswa amepata fursa hiyo katika Kongamano la Mawaziri wanaosimamia Sekta za Madini kwa nchi za Afrika zinazotarajia kushiriki Mkutano wa Uwekezaji wa Mining Indaba unaoanza Februari 5 hadi 8, 2024, Capetown nchini  Afrika Kusini ambao mwaka huu unatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza katika kongamano hilo, Dkt. Kiruswa  ameeleza hatua mbalimbali  ambazo Serikali  ya Tanzania  imeendelea  kuzichukua  katika uendelezaji wa madini muhimu na mkakati na kuielezea    miradi ya uchimbaji na uchakataji wa madini ya nikeli unaotekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Tembo Nikel na miradi ya uchimbaji madini ya graphite ambayo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Halikadhalika, Dkt. Kiruswa  ameeleza kuhusu uwepo wa  masoko ya  madini  yapatao 42 na vituo vidogo vya ununuzi  madini  vipatavyo 96 yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali  nchini na namna ambavyo masoko hayo yameongeza uwazi, tija  na kurahisisha biashara  ya madini kwa Tanzania.

Ameongeza  kuhusu uwepo wa mfumo wa uombaji leseni  za madini ambao  umeongeza  uwazi kwa waombaji wa leseni  za madini na  kueleza namna ambavyo Serikali inaamini  katika kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza sekta za madini.

‘’ Tunajua kuwa tunahitaji  kushirikiana na wawekezaji ili tuwe pamoja na kuwa na sauti moja,’’amesema Dkt.Kiruswa.

Pia, ameeleza kuhusu umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika uchumi wa Madini na kuieleza hadhira hiyo juu ya jitihada ambazo zimefanywa na Serikali ya Tanzania kurasimisha  shughuli za uchimbaji mdogo wa madini ambapo mchango wao katika maduhuli  ya Serikali umeongezeka na kufikia asilimia 40.

Mbali na kutoa uzoefu huo, Dkt. Kiruswa amezinadi fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta yaMadini Tanzania na kuzitaja kuwa ni pamoja na  utafiti wa madini  hususan madini mkakati, uongezaji thamani madini pamoja na kueleza mazingira rafiki ya biashara yaliyopo katika Sekta ya Madini ikiwemo  Sheria, Sera na Kanuni zinazosimamia sekta ya madini nchini ambapo pia amevitaja vipaumbele vya Serikali katika kuendeleza Sekta ya Madini.

Wakizungumza katika ufunguzi wa  kongamano hilo kwa nyakati tofauti,  Waziri wa Nishati na Madini wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Gwane Mantasha amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali za Afrika na kusisitiza umuhimu wa madini  kuongezwa thamani ndani ya bara la Afrika.

Naye,  Rais wa  Taasisi ya Jiolojia ya Afrika Kusini Norera Fakude amezitaka nchi  za Afrika kuiona  na kuifanya kesho ya Afrika  kuwa sasa  na kuhakikisha rasilimali madini zinazinufaisha  bara hilo sasa na wakati mwingine.

Katika Kongamano hilo, mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwemo masuala yanayohusu teknolojia, kushirikishana ujuzi na uzoefu na umuhimu wa kutumia viwanda vya uongezaji thamani madini vya ndani ya bara hilo.

Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo kwa mwaka huu umekuwa wa pamoja tofauti na miaka mingine ambapo Wizara ya Madini imeshirikiana na Chemba ya Migodi kuwezesha ushiriki huo. Tanzania katika mkutano huo inatarajia kushiriki katika shughuli mbalimbali kuendelea kuzinadi fursa zake za kiuwekezaji katika Sekta ya Madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *