MBUNGE DKT. CHAYA AKABIDHI GARI JIPYA LA KUBEBEA WAGONJWA KINTINKU MANYONI.
Na: Emmanuel Charles, Manyoni- Singida
Wananchi wa Tarafa ya Kintinku Wilayani Manyoni Mkoani Singida wataondokana na adha ya kushindwa kukimbizwa Hospital kwa haraka baada ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwapatia gari la kubebea wagonjwa(Ambulance).
Mbunge wa Manyoni Mashariki Mhe. Dkt. Pius Chaya amekabidhi gari hilo leo Februari 05, 2024 katika Kituo cha Afya Kintinku.
Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo mbele ya wananchi na Viongozi wa Wilaya ya Manyoni Mbunge Dkt. Chaya amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa gari hilo ambalo litakwenda kuondoa adha hususani ya akina Mama katika Jimbo hilo na Tarafa ya Kintinku waliokuwa wakipata tabu wakati wa kujifungua kwa kushindwa kukimbizwa Hospital kwaajili ya kupatiwa huduma kwa haraka.
“Huku bondeni tuna vituo vya Afya viwili, Kintinku na Chibumagwa Nategemea hii ambulance vile vile itaokoa akina Mama ambao watashindwa kujifungua kituo cha Afya cha Chibumagwa lakini itakaa Kintinku lakini itasaidia wagonjwa wote wa Tarafa ya Kintinku.”
“tunataka Mama atakayeshindwa kujifungua kutoka Mahaka, Mama atakayeshindwa kujifungua kutoka Chikuyu, Makutupora, Makanda hii gari iwepo kwaajili ya kuokoa uhai wa Mama” amesema Mbunge Dkt. Chaya
Ameeleza kuwa gari hiyo itanusuru akina Mama na watoto, na wagonjwa ambao wanahitaji kukimbizwa Dodoma au Manyoni
Ametoa wito kwa Mganga Mkuu kuhakikisha gari hiyo inatoa huduma kwa wananchi wote bila ubinafsi kwani lengo ni kuokoa uhai wa Mama na Mtoto na kuwasaidia wananchi kuwa na Afya Bora.
Kwa Upande wao wananchi wamemshukuru Rais Samia na Mbunge Dkt. Chaya kwa kuwapatia gari hilo.
Baadhi ya akina Mama wakiwa katika furaha kubwa wamesema walikuwa wakipata shida na wengine kupoteza maisha lakini uwepo wa gari hilo utakwenda kusaidia kuondokana na tatizo hilo.
“2025 tumtangulize Mama Samia kwa kura nyingi, kwakweli Mama wajawazito tulikuwa tunahangaika tunajizalia njiani, tunamshukuru Mama kwa kutuletea hii gari” wamesema wananchi hao.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni katika tukio hilo ambaye ni Mfamasia wa Halmashauri ya Manyoni Alfred Burchard Rwamtoga amesema kukosekana kwa gari hilo la wagonjwa imekuwa ni adha kubwa na ya muda mrefu na kusababisha shida ya kusafirisha wagonjwa wa dharula hivyo wanamshukuru Rais Samia kwa kuwapatia gari hilo ambalo anaamini litakwenda kuokoa maisha ya wananchi.
“Gari hili tukilitumia vizuri litakwenda kuleta mafanikio makubwa ya kuokoa maisha ya watoto wachanga, wajawazito na wagonjwa wengine ambao watahitaji kupewa Rufaa ambapo kwa sasa wataweza kwenda Dodoma, Manyoni, St. Gaspar Itigi na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.” Amesema Mwakilishi huyo.
Aidha, Diwani wa Kata ya Kintinku Joseph Julius amemshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwajali wananchi na kuendelea kufikisha miradi katika maeneo mbalimbali nchini.
Ikumbukwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni ametoa magari zaidi ya mia mbili ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Gari jipya la kubebea wagonjwa Kituo cha Afya Kintinku, Manyoni.
Gari la Zamani la kubebea wagonjwa Kituo cha Afya Kintinku, Manyoni.