TEHAMA KUBORESHA ELIMU NCHINI – DKT. MSONDE
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde amesema Serikali imetoa vifaa vya TEHAMA kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (Boost) ili kuboresha mafunzo endelevu ya walimu kazini na wanafunzi kujifunza.
Akizungumza leo kwenye uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya TEHAMA kwa vituo vya walimu (TRC) wa shule za Msingi na Awali jijini Dodoma vilivyogharimu Sh.Bilioni 6.9, Dkt.Msonde amesema kuwa walimu watakuwa na uwezo wa kufundisha kupitia mtandao kwa kutumia TEHAMA jambo ambalo litasaidia kuboresha elimu nchini.
“Vifaa hivi vitawawezesha wanafunzi kusoma na mwalimu mmoja anaweza kufundisha somo moja kwa wanafunxi wa shule mbalimbali kwa kutumia TEHAMA, hii itasaidia hasa maeneo yenye upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kuweza kufundisha kwa shule ambayo haina mwalimu kupitia TEHAMA,” amesema Dkt.Msonde
Amesema kuwa ni malengo ya Serikali katika kuhakikisha inaboresha elimu kwa kuboresha elimu kwa kujenga miundombinu bora na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.