WENGINE 600 WAHAMA KWA HIARI HIFADHI YA NGORONGORO

0

Na Richard Mrusha  Arusha

Serikali imelipongeza kundi la watu 600 waliokuwa wakazi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwa uamuzi wao wa  hiari wa kupisha shughuli za uhifadhi ndani ya hifadhi hiyo.


Pongezi hizo zimetolewa leo  Februari 1, 2024 na Kamishina wa Uhifadhi  wa Ngorongoro, Richard Kiiza wakati akiliaga kundi hilo lililoanza safari majira ya saa 12:30 asubuhi kutokea ofisi ya zamani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Msomera.

“Ndugu zangu nawashukuru kwa hamasa kubwa mliyonayo Sasa ya kuanza  kuondoka kwa hiari hifadhini kupisha uhifadhi maana sasa spidi ya kujiandikisha imekuwa kubwa  katika kipindi kifupi” amefafanua Kamishina Kiiza.

Amewahakikishia kuwa dhamira ya Serikali ni njema ya kutaka kuboresha maisha yao na kuwaomba  wawndelee kuwashawishi wenzao  waliobaki ili pia waboreshe maisha yao.

Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele ambaye  pia ndiye Msemaji wa Wizara hiyo anasisitiza” Nimefarijika kuona wananchi wanaofurahia maisha wakifika Msomera wamekuwa mabalozi wazuri wa kuwaelezea jinsi Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ilivyoboresha maisha yao”

Hadi sasa kundi hili linakuwa kundi la tano kwenda eneo la Msomera ikiwa ni jumla ya kaya 934 zenye jumla ya watu 5747 na mifugo 26227.

Serikali imekuwa ikizingatia haki zote za msingi wakati wa kuwahamisha wananchi wanaopisha uhifadhi kwa hiari ikiwa ni pamoja na kujengewa nyumba bure, kulipwa fidia ya  maendelezo,  kupewa shamba  la ekari tano, kifuta jasho cha milioni kumi, kusafirishwa wao na mizigo yao na kuendelea kupatiwa mahindi kwa ajili ya chakula kwa mwaka mmoja na nusu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *