TADB YAONGEZA NGUVU UTOAJI WA MIKOPO KWA WAKULIMA

0

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia mfuko wa dhamana ya wakulima wadogo (SCGS) imeingia makubaliano ya kuongeza mkataba wa ushirikiano na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwa ajili ya utoaji dhamana ya mikopo ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Akizungumza leo february 1, 2024 jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kutia sahihi,  Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Frank Nyabundege, amesema kuwa makubaliano hayo utaiwezesha TADB kuchagiza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima kupitia TCB.

“Watatoa mikopo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi na TADB itatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa mikopo yote hususani kwa vijana, wanawake na miradi inayosaidia kupungunza au kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi” amesema Bw. Nyabundege.

Amesema kuwa wanufaika  wengine wa mikopo ni  wachakataji wa mazao wadogo na wakati, wakulima pamoja na wafugaji wa mifugo na uvuvi.

Bw. Nyabundege amesema kuwa wameingia makubaliano na TCB kwa sababu wanafanya kazi nzuri hasa kuendelea kuchagiza maendeleo ya kilimo nchini kupitia matawi yao ambayo yapo katika mikoa yote ya Tanzania.

Amesema kuwa ushirikiano na TCB ulianza mei mwaka 2018 na kuleta tija na manufaa kwa wakulima na sekta ya Kilimo nchini.

Amefafanua kuwa Mkataba wa awali ambao umemalizika kupitia dhamana ya TADB, TCB ilitoa jumla ya shilingi bilioni 34.1 kwa wanufaika wa moja kwa moja 2,638 na wasio wa moja kwa moja zaidi ya 7,750.

Amesema zaidi ya asilimia 95 ya wanufaika ni wakulima wadogo na wajasiriamali wadogo wa vijijini wanaoshughulika na mnyororo wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha TADB kutimiza majukumu yake kwa ufanisi na kuleta tija kwa Taifa” amesema
Bw. Nyabundege.

Afisa Mtendaji Mkuu Benki ya Biashara Tanzania (TCB) Bw. Adam Mihayo, amesema kuwa kupitia makubaliano hayo TCB itaongeza wigo wa kutoa mikopo na kuwafikia wakulima katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kwa kuwapatia mitaji itakayo wawezesha kutoka katika kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha biashara kwa riba nafuu.

“Tunaishukuru TADB, na mikopo hii inapatikana katika matawi yote ya TCB yaliyopo Tanzania, lengo la kuongeza mkataba huu ni kuhakikisha tunawafikia wakulima wote nchini kwa kuwaongezea mitaji itakayowawezesha kufanya kilimo Cha biashara ili kujikwamua kiuchumi” amesema Bw. Mihayo.

TCB kushirikiana na TADB unafanya Jumla ya taasisi za kifedha zinazonufaika na Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS) na kufikia 16.

Taasisi hizo zinajumuisha Benki ya za Biashara, Benki za Kijamii na Taasisi ndogo za fedha (Microfinance Financial Institutions) zenye uwezo wa kuhudumia wakulima kupitia mtandao wa matawi zaidi ya 700 nchini.

Mpaka kufikia Desemba 2023 TADB kupitia SCGS imetoa shilingi bilioni 250.77 kwa wanufaika wa moja kwa moja zaidi ya 19, 400 na wasio wa moja kwa moja zaidi ya 897,900 kutoka mikoa 27 ( asilimia 87 ya mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani) ambapo zaidi ya asilimia 95 ya wanufaika Wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *