BARABARA YA KIDATU-IFAKARA NA DARAJA LA RUAHA

KUKAMILIKA MACHI
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemtaka
mkandarasi Reynolds Construction Company (RCC), anayejenga
barabara ya Kidatu- Ifakara km 66.9 na daraja la Ruaha lenye
urefu wa mita 133 kuhakikisha ujenzi wa barabara na daraja hilo
unakamilika ifikapo Machi mwaka huu.
Kukamilika kwa daraja hilo linalounganisha wilaya za Kilosa na
Kilombero mkoani Morogoro kutafungua uchumi wa wakazi wa
mikoa ya Morogoro, Njombe, Iringa na Ruvuma kwa kuwa inapita
kwenye eneo lenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na
biashara.
“Kwa kuwa katika ujenzi huu hakuna changamoto ya fedha hivyo
katika miezi miwili ijayo hakikisheni kazi hii inakamilika na
wananchi wananufaika na uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na
Serikali”, amesema Eng. Kasekenya.
Amezungumzia umuhimu wa Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), kushirikiana na mkandarasi kuhakikisha alama
muhimu za usalama barabarani zinawekwa mapema
iwezekanavyo ili kuepusha ajali kwa watumiaji wa barabara hiyo
na kuhakikisha magari yatakayotumia barabara hiyo hayazidishi
uzito.
Kwa upande wake meneja wa TANROADS mkoa wa morogoro
Lazeck Kyamba amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa
watamsimamia mkandarasi huyo ili kazi zifanywe usiku na
mchana na hivyo kukamilika katika muda mfupi ujao.
Nae mkuu wa wilaya ya Kilombero Dastan Kyobya amesema
kukamilika kwa daraja la ruaha na barabara hiyo kutaleta fursa
nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa wilaya hiyo na kuipongeza
TANROADS kwa usimamizi mzuri na shirikishi kwa wananchi.
Katika hatua nyingine naibu waziri kasekenya amekagua
barabara ya mikumi-kilosa hadi dumila ambayo ujenzi wake
unaendelea kwa awamu na kumtaka mkandarasi Umoja JV
anaejenga sehemu ya Rudewa-Kilosa km 22.5 kukamilisha
madaraja matatu ya Mazinyungu, Kobe na Wailonga yaliopo mjini
Kilosa ili kukamilisha mradi huo na kuwawezesha wananchi
kunufaika na mradi huo.
Naibu Waziri Kasekenya yuko mkoani Morogoro kukagua
maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja
na kusisitiza umuhimu wa watumiaji wa barabara kuzingatia
sheria ili kuilinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu.